Je, Mbona Sheria zetu humu nchini hazijatafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili?

Kwa muda sasa, nimekuwa nikitafakari kuhusu nafasi ya Ibara ya 7 ya Katiba ya Kenya inayotambua Kiswahili kama lugha rasmi ya Jamhuri yetu (pamoja na Kiingereza). Nimekuwa nikijiuliza ni kwa nini sheria zetu za Kenya hazijatafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili, miaka tisa baada ya kuzinduliwa kwa Katiba yetu.

Ili kupata jibu, nimekuwa nikisoma tasnifu (thesis) ya Njenga Grace Waithira ya kutosheleza baadhi ya mahitaji ya shahada ya uzamili wa sanaa (Kiswahili) katika Chuo Kikuu Cha Nairobi. Mada ya tasnifu yake ni “Changamoto za Kutafsiri Matini za Kisheria: Tathmini ya Katiba ya Kenya (2010)”.

Katika ikisari ya tasnifu, dada Grace anaeleza kuwa kutafsiri matini za kisheria huwa na changamoto nyingi. Changamoto hizi husababishwa na sifa za kiisimu kama vile leksia, sintaksia, semantiki na pragmatiki. Kunayo mambo mengine ambayo si ya kiisimu kama vile tofauti za tamaduni za jamii husika na tofauti za kihistoria ambazo pia huzua changamoto katika kutafsiri matini za kisheria.

Grace anatathmini sura ya kumi na moja ya katiba ya Kenya na kutoa mifano mahsusi ya changamoto hizi kama zinavyojitokeza katika sura hii. Mifano yake ni mingi tu.

Katika hitimisho, Grace anaandika haya:

Uchunguzi wetu umedhihirisha kuwa ukosefu wa ulinganifu wa kiistilahi ni mojawapo ya changamoto mtafsiri wa kisheria hukumbana nayo. Kwa vile maana hubebwa katika misingi wa kiisimu ya leksia ,sintaksia na semantiki, ukosefu wa ulinganifu wa kiistilahi hujitokeza katika ngazi hizi za kiisimu na huleta upotoshi wa kimaana.

Naomba tena kunukuu mapendekezo yake mengine:

Jambo lingine ambalo tulipata kujua katika utafiti wetu ni kuwa kutafsiri sheria si jambo rahisi. Sheria ni taaluma ambayo ina istilahi zake maalum na kaida zingine za kisheria ambazo mtu wa kawaida huenda asielewe. Ili kuweza kupata ufanisi katika kutafsiri matini za kisheria, mtafsiri anafaa kuwa na ujuzi wa kimsingi katika masuala ya kisheria. Kwa hivyo watafsiri wa matini za kisheria wanafaa angalau wapate elimu ya kisheria hata kama ni ya kimsingi. Aidha walio na elimu ya kisheria nao wanaweza kushirikishwa katika shughuli za kutafsiri matini za kisheria. Wanaweza kupewa elimu ya kimsingi ya kiisimu ili waweze kuimudu kazi hii ya kutafsiri matini za kisheria.

Lakini tusikate tamaa, kwani jambo hili linawezekana. Mapendekezo yangu kwa taifa la Kenya ni haya:

1. Kuwe na sera ya kutafsiri matini za kisheria kutoka Kiingereza (lugha chanzi) hadi Kiswahili (lugha lengwa). Mwanasheria Mkuu, Jaji Kihara Kariuki, kazi kwako.

2. Hatua kabambe ichukuliwe na Bunge la Kenya (Bunge la Taifa na Seneti) ili kutafsiri sheria.

3. Somo la Kiswahili lazima lisisitizwe katika silabasi za vyuo vikuu na somo la Kiswahili la lazima liwepo haswa katika taaluma ya sheria.

4. Uchapishaji wa Makala na vitabu kwa lugha ya Kiswahili, hususan katika taaluma ya sheria, usisitizwe na kuwe na miradi thabiti za serikali za kuwazawadi na kuwapiga jeki wanaotia juhudi.

5. Taasisi za elimu hapa Kenya zishirikiane na taasisi za elimu za majirani zetu Watanzania ili kukuza kipaji cha Kiswahili. Pia, kuwe na programu za kuwasafirisha wanafunzi kule ili wafaidi katika kukuza Kiswahili.

6. Wahadhiri wa Kiswahili wa vyuo vikuu na Shule za Upili washirikishwe zaidi kupitia sera niliyotaja hapo juu katika uwanja huu wa utafsiri, haswa wa matini za sheria.

 

ayes & nays

Spread the love