Mswada wa Kudhibiti Michango

Kuna Mswada katika Bunge la Taifa utakaodhibiti suala hili la michango au harambee. Jina la Mswada ni Public Fundraising Appeals Bill.

Kuna vifungu kadhaa ambavyo nitavitaja upesi upesi:

1. Ikiwa utataka kuendesha harambee ambayo inahusisha umma, basi utafaa kupata leseni au kibali kutoka kwa Mamlaka ya Polisi katika Kaunti (County Policing Authority). Mamlaka hii ina wanachama takriban 13 nao ni Gavana ambaye ni Mwenyekiti, Mwakilishi kutoka Idara ya Taifa ya Ujasusi, Mkuu wa Polisi na Idara ya Upelelezi katika Kaunti, Wawakilishi wa Baraza la Kaunti wawili, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama katika Kaunti na wanachama saba watakaoteuliwa na Gavana.

2. Ombi la leseni lazima iwasilishwe kwa Mamlaka ya Polisi katika Kaunti siku 21 kabla ya kuendesha mchango.

3. Fungu la kumi, zaka na pesa zinazokusanywa ndani ya mifumo ya madini yetu hayatahitaji leseni. Pia, pesa za uanachama katika vyama au mashirika hayatahitaji leseni kwa mujibu wa sheria hii. Kuna masuala mengine sijataja.

4. Michango ya familia hayatahitaji leseni. Lakini pindi tu utakapopania kuhusisha wengine wasio wa familia yako, utafaa kuwasilisha ombi la leseni.

5. Mbunge (awe Mbunge wa Bunge la Taifa au Seneta) na Mwakilishi wa Baraza la Kaunti (MCA) hawatashiriki au kuendesha michango au harambee katika hatamu zao. Adhabu ya kukiuka kifungu hiki ni faini ya kima kisichozidi 800,000/=

6. Ombi la leseni litakuwa na masuala haya:
– Jina na anwani ya anayenuia kuendesha mchango
– Sababu ya mchango
– Umuhimu wa mchango
– Tarehe ya mchango
– Majina na habari za simu, anwani n.k. za wasaidizi wa kuendesha mchango
– Kiasi cha fedha kinachonuiwa kukusanywa
– Makadirio ya matumizi katika kuendesha mchango
– Kauli iwapo pesa zimepokelewa kabla ya mchango kuendeshwa
– Mahali paliponuiwa kuendesha mchango
– Muda wa kuendesha mchango
– Habari nyingine yoyote ile ya muhimu

7. Ukishaendesha mchango, ngoma haijaisha. Unafaa kuhifadhi rekodi zinazohusiana na mchango ikiwemo waliochanga; jina, namba za akaunti na anwani za benki pesa ziliwekwa; habari kamili ya fedha na mali zilizokusanywa, habari kamili ya matumizi ya fesha na mali zilizokusanywa; habari ya pesa zilivyotumika kuandaa na kuendesha mchango pamoja na mishahara. Rekodi hizi zinafaa kuwasilishwa kwa Mamlaka ya Polisi katika Kaunti ndani ya siku 30 baada ya mchango kuendeshwa.

8. Mswada unapendekeza kuwe na wakaguzi au inspectors ambao wataweza kukagua rekodi na habari za hasibu au hata kuzichukua.

9. Mswada unapendekeza kuwa anayetoa mchango lazima atataja kiini cha mchango wake, yaani pesa kazitoa wapi na kutaja pesa hizi anapowasilisha fomu za malipo ya ushuru.

10. Mswada unapendekeza kuundwa kwa Kamati ya Kitaifa ya Michango, yaani Public Fundraising Appeals Committee, itakayotoa usimamizi wa michango katika kiwango cha kitaifa na kuchunguza malalamishi, matumizi mabaya ya fedha zilizokusanywa katika michango au jambo lolote ile.

11. Sheria ina makali, si butu. Ukivunja sheria hii, utalimwa na kifungo cha miaka zisizodi mitano au utozwe faini zisizozidi milioni mbili.

12. Mswada huu unatengua sheria iliyopo ya Udhibiti wa Michango ya Umma, yaani Public Collections Act (Sura ya 106 ya Sheria za Kenya).

Mswada huu umedhaminiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Utekelezaji wa Katiba, Mhe. Jeremiah Kioni. Hatua ya uhusishaji wa umma (public participation) umekamilika. Maoni yakishakusanywa, kamati itawasilisha ripoti yake na Mswada utavukishwa hadi hatua zingine za Mswada Kusomwa Mara ya Pili (Second Reading) na Kamati ya Bunge Zima  ambapo marekebisho yatapendekezwa na kupitishwa kisha iwasilishwe Seneti ili nao washughulikie Mswada huu.

Unaweza kupakua nakala ya Mswada huu kwa kubonyeza tovuti ya Bunge la Kenya.

ayes & nays

Spread the love