Marekebisho katika Toleo la 6 la Kanuni za Kudumu za Bunge la Taifa

Utangulizi

Bunge linaendeshwa na kanuni, mazoea, mitindo, uamuzi wa awali, desturi, taratibu, mila na mienendo yake na mabunge mengine. Kanuni za Kudumu zinatoa mwelekeo wa jinsi ambavyo shughuli za Bunge zitaendeshwa katika ukumbi na kamati. Kanuni za Kudumu, au Standing Orders, katika lugha ya Kiingereza, zinatoa majibu kwa kiasi kikubwa ya maswali ambayo viongozi wa kikao na wabunge wanaweza kuwa nayo kuhusu taratibu za Bunge.

Marekebisho ya Kanuni za Kudumu yamekuwa yakifanywa tangu tulipojinyakulia uhuru. Makala haya yataangazia marekebisho ambayo yalifanywa katika kipindi cha sita cha Bunge la awali la kumi na mbili.

Marekebisho

Jopo la Mwenyekiti kuongezwa toka wajumbe 4 hadi 6

Awali, Jopo la Mwenyekiti lilikuwa na Wajumbe wanne. Hivi sasa, idadi imeongezwa hadi Wajumbe sita. Hivyo, Jopo la Mwenyekiti lina Wajumbe sita watakaotambulika kama Mwenyekiti wa Kwanza, wa Pili, wa Tatu, wa Nne, wa Tano na wa Sita mtawalia na watatekeleza mamlaka yote ya Mwenyekiti wa Kamati.

Muda wa kushughulikia uteuzi wa maofisa wa umma kuongezwa toka siku 14 hadi 21

Baada ya kupokea taarifa ya uteuzi kwa Ofisi ya Serikali au ofisi nyingine yoyote kwa mujibu wa Katiba au sheria nyingine unaotaka kuidhinishwa na Bunge, uteuzi huo unafaa kukabidhiwa Kamati ya Kiidara inayohusika ili ushughulikiwe.

Kanuni inaeleza kuwa Kamati itafanya kikao kwa ajili ya kushughulikia uteuzi uliopendekezwa na isipokuwa kama imeelezwa vinginevyo katika sheria, itawasilisha ripoti yake kwa Bunge la Taifa katika muda usiozidi siku ishirini na moja baada ya kukabidhiwa taarifa ya uteuzi. Awali muda huu ulikuwa siku kumi na nne.

Hoja ya Kipekee ya Risala za Bunge la Taifa kutolewa bila arifa

Kanuni ya 52 inaorodhesha Hoja zinazoweza kutolewa bila arifa. Kanuni hii ilirekebishwa ili kuongezea Hoja ya kipekee ya risala za Bunge la Taifa kwa mujibu wa Kanuni ya 259D (Risala za Bunge).

Marufuku kurejelea dondoo kutoka katika magazeti au vyombo vya habari vya kielektroniki kama rejeleo rasmi katika hotuba

Kanuni ya 87 imerekebishwa ili kupiga marufuku  kule Mbunge kurejelea dondoo kutoka katika magazeti au vyombo vya habari vya kielektroniki kama rejeleo rasmi katika hotuba yake.

Muda wa kutosha wa kujadili Mswada wa kurekebisha Katiba

Bunge la Taifa linaweza kudhibiti mjadala kuhusu Hoja au Mswada kwa kutenga muda wa mjadala huo au kwa kudhibiti muda ambao Wabunge wanaweza kuchangia mjadala huo au kwa kuweka vidhibiti vinginevyo, kufuatia Hoja iliyotolewa na Mbunge yeyote kwa mujibu wa Kanuni hii.

Kanuni ya 97 imerekebishwa ili Wabunge wanaopenda kujadili Mswada wa kurekebisha Katiba wapate fursa ya kutosha ya kufanya hivyo bila ya wengi wa wabunge kufunga mjadala wakati wowote.

Udhamini wenza wa mapendekezo ya miswada na miswada

Kanuni ya 114 sasa inaruhusu udhamini wenza wa mapendekezo ya miswada na miswada. Kwa mfano, ikiwa Wabunge wawili wangependa kudhamini pendekezo la mswada au mswada, majina yao yataandikwa katika pendekezo la mswada au mswada huo.

Muda wa uchanganuzi wa pendekezo la mswada kabla uchapishaji umeongezwa toka siku 21 hadi 30

Uchanganuzi wa pendekezo la mswada kabla uchapishaji ni mchakato unaohusu Kamati ya Kiidara kutathmini pendekezo la mswada ili kubaini ikiwa linafaa kuchapishwa kama mswada. Kimsingi, Kamati huuliza maswali kama yafuatayo:

Je, pendekezo hili ni thabiti haswa katika sera?

Je, kuna mkinzano baina ya pendekezo hili na sheria nyinginezo?

Je, sheria hii ni nzuri?

Katika toleo la awali la Kanuni za Kudumu, muda wa kufanya haya uliokuwa siku 21. Kwa sasa, muda huu umeongezwa hadi siku 30.

Maelekezo kuhusu pendekezo la Mswada wa kurekebisha Katiba

Kanuni ya 114 imerekebishwa ili kutoa maelekezo kuhusu pendekezo la Mswada wa kurekebisha Katiba. Haya ndiyo mabadiliko:

 • Pendekezo litaambatanishwa na saini za angalau Wabunge wasiopungua 50 wanaoiunga mkono, isipokuwa kama imedhaminiwa na Chama cha walio Wengi au Chama cha walio Wachache
 • Pale ambapo Spika anaidhinisha uchanganuzi kabla ya kuchapishwa kwa pendekezo, Spika ataliarifu Bunge la Taifa kuhusu idhinisho hilo na anaweza—

— kumruhusu mdhamini atoe kauli ya madhumuni na sababu za pendekezo

— kuruhusu maoni yatolewe kuhusiana na kauli iliyotolewa na Mbunge

— kuwezesha kujumuishwa kwa maoni ya wabunge katika baraza faafu

— kuwaalika Wabunge walio na mapendekezo yanayofanana au yanayohusiana kutoa mawasilisho yao mbele ya Kamati inayokabidhiwa pendekezo

 • Baraza au kamati inayokabidhiwa pendekezo la Mswada—

  — itaalika na kushughulikia mawasilisho ya Mwanasheria Mkuu; tume na ofisi huru zilizoundwa kwa mujibu wa Sura ya kumi na tano ya Katiba na asasi yoyote ya kikatiba au kisheria iliyo na wajibu wa kurekebisha sheria

— kwa kushauriana na mdhamini, itajitahidi kuandaa na kupendekeza nakala patanifu ya pendekezo kutokana na mawasilisho yaliyopokewa

 • Kufuatia maoni ya Kamati ya Kiidara inayohusika, Spika ataelekeza pendekezo la mswada lichapishwe au lisichapishwe kuwa mswada

Pendekezo la mswada kutoka kwa chama kinachounda Serikali ya Taifa au Tume ya kikatiba au Ofisi Huru na linahusiana na wajibu wa Tume au Ofisi Huru kutopitia mchakato wa uchanganuzi wa pendekezo la mswada kabla ya uchapishaji

Kanuni ya 114A inaeleza kwamba Spika anaweza kuruhusu pendekezo la mswada lisifuate masharti ya Kanuni ya 114 (Uwasilishaji wa Miswada) ikiwa linatoka kwa chama kinachounda Serikali ya Taifa au Tume ya kikatiba au Ofisi Huru na linahusiana na wajibu wa Tume au Ofisi Huru.

Pia, ruhusa hii itatolewa kwa pendekezo linalokusudia kutekeleza uamuzi wa Bunge au pendekezo la Kamati ya Ardhilhali za Umma, kutekeleza, kurekebisha au kufuta sheria yoyote; au pendekezo linalofanana na Mswada uliopitishwa na Bunge la Taifa lakini ukatanguka mwishoni mwa muhula wa Bunge lililotangulia; au liliwasilishwa na Mbunge yuyo huyo na likasomwa kwa mara ya pili lakini likatanguka mwisho wa muhula wa Bunge lililotangulia.

Ruhusa haitatolewa isipokuwa kama pendekezo la mswada limeambatishwa na nakala ya idhini ya Baraza la Mawaziri, ikiwa pendekezo la mswada limetolewa na Chama kinachounda Serikali ya Taifa; au sera iliyo msingi wa pendekezo la mswada na ushahidi wa mashauriano ya wadau, ikiwa pendekezo limetolewa na Tume au Ofisi Huru.

Chama kinachounda Serikali ya Taifa kitataja jina la Mbunge atakayewasilisha pendekezo la mswada ili lichapishwe.

Baada ya ruhusa kutolewa, Spika ataamuru pendekezo hilo la mswada lichapishwe kuwa mswada.

Rekebisho la Kanuni ya 121 ili ioane na Ibara ya 110(3) ya Katiba

Kanuni ya 121 imerekebishwa ili kueleza kwamba kwa mujibu wa Ibara ya 110(3) ya Katiba, kabla ya Bunge la Taifa au Seneti kushughulikia Mswada, Spika wa Bunge la Taifa na Spika wa Seneti wataamua kwa pamoja iwapo ni Mswada unaohusu kaunti, na ikiwa ni hivyo, kama ni Mswada maalum au Mswada wa kawaida.

Muda wa kuwasilisha ripoti kuhusu mswada imeongezwa toka siku 21 hadi 30

Kanuni ya 127 imefanyiwa marekebisho hivyo basi Mwenyekiti wa Kamati ya Kiidara ambayo imekabidhiwa Mswada au mjumbe wa Kamati aliyeteuliwa kwa ajili hiyo anafaa kuwasilisha ripoti ya Kamati katika Bunge la Taifa  kwa muda usiozidi siku 30 za kalenda baada ya kukabidhiwa Mswada ili kuboresha mjadala.

Mbunge hawezi kuondoa mswada unaokusudia kutekeleza uamuzi wa Bunge au pendekezo la Kamati ya Ardhilhali za Umma, kutekeleza, kurekebisha au kufuta sheria yoyote bila idhini ya Spika

Kanuni ya 140 inaeleza kwamba kabla ya shughuli kuanza au wakati wa kusoma shughuli hiyo kwenye Ratiba ya Shughuli katika hatua yoyote kwa Mswada kusomwa, Mdhamini wa Mswada anaweza kuomba kuondoa Mswada bila kutoa arifa. Iwapo kwa maoni ya Spika ombi linalotolewa halihujumu shughuli za Bunge la Taifa, ataelekeza Mswada uondolewe.

Kanuni hii imerekebishwa. Hivyo basi, mswada unaokusudia kutekeleza uamuzi wa Bunge au pendekezo la Kamati ya Ardhilhali za Umma, kutekeleza, kurekebisha au kufuta sheria yoyote unaweza kuondolewa tu kwa idhini ya Spika.

Kanuni ya 142 inayohusu maafikiano na Seneti kufutwa na kubadilishwa ili kuelezea utaratibu wa udhamini wenza wa mswada

Kanuni ya 142 inaeleza kwamba pale ambapo Mswada, isipokuwa Mswada ambao kwa mujibu wa Ibara ya 109(3) ya Katiba unastahili kushughulikiwa na Bunge la Taifa pekee, umepitishwa Mdhamini wa Mswada huo, katika muda usiozidi siku saba, atamjulisha Spika kwa maandishi jina au majina ya Mbunge au Wabunge wowote wa Seneti ambao amewateua kuwa wadhamini wenza wa Mswada huo katika Seneti. Katibu wa Bunge la Taifa atawasilisha kwa Katibu wa Seneti nakala ya Mswada iliyothibitishwa, kwa kutiwa saini na Katibu na kuidhinishwa na Spika, ikiambatana na Ujumbe wa kuomba maafikiano ya Seneti na ukiiarifu Seneti jina la Mbunge au Wabunge wa Seneti walioteuliwa kuwa wadhamini wenza wa Mswada huo.

Udhamini wenza kujumuishwa katika utaratibu wa kushughulikia miswada inayoanzia Seneti

Sawa na Kanuni ya 142, Kanuni ya 143 imerekebishwa ili kuchopeka dhana ya udhamini wenza. Kanuni sasa inaeleza kwamba kila mara Spika anapopokea Mswada unaoanzia Seneti atalifahamisha Bunge la Taifa kupitia Ujumbe, atalifahamisha Bunge la Taifa jina la Mbunge au Wabunge walioteuliwa na Mdhamini wa Mswada kuwa wadhamini wenza wa Mswada huo katika Bunge la Taifa na ataelekeza Mswada huo usomwe Mara ya Kwanza.

Baada ya kusomwa Mara ya Kwanza, Mswada utakabidhiwa Kamati husika na Mswada huo utashughulikiwa kwa namna ileile kama Mswada unaoanzia katika Bunge la Taifa.

Orodha ya marekebisho kutumwa Seneti

Kanuni ya 144 inaeleza kuwa pale ambapo Mswada unaoanzia katika Seneti umesomwa Mara ya Tatu katika Bunge la Taifa, Katibu ataelekeza rekebisho au marekebisho yoyote ambayo yamefanywa katika Mswada huo katika Bunge la Taifa kujumuishwa kwenye Mswada uliopokelewa kutoka Seneti na nakala ya Mswada iliyorekebishwa na orodha ya marekebisho, iliyotiwa saini na Katibu na kuidhinishwa na Spika, itarejeshwa kwa Seneti ikiambatisha Ujumbe wa kutaka maafikiano na Seneti kuhusu rekebisho au marekebisho ya Bunge la Taifa.

Kanuni mpya kuhusu kuridhia mikataba

Kanuni mpya ya 170A imeongezwa inayohusu kuridhia mikataba. Kanuni hii inaeleza kwamba Mkataba uliowasilishwa katika Bunge la Taifa ili uridhiwe utawasilishwa katika Meza ya Bunge na kukabidhiwa Kamati husika ili ushughulikiwe. Kamati husika itashirikisha umma kabla ya kutoa ripoti yake katika Bunge la Taifa.

Pamoja na taarifa inayohitajika kutolewa katika Bunge la Taifa kwa mujibu wa sheria, Kamati inaweza kumhitaji Waziri husika kutoa taarifa zaidi, ikijumuisha athari ya kijamii na kimazingira ya mkataba huo katika muda mfupi, muda wa wastani na muda mrefu; na,aina na ushahidi wa ushirikishwaji wowote wa umma uliofanywa kuhusu mkataba huo.

Ripoti ya Kamati husika kwa Bunge la Taifa itajumuisha taarifa ya maoni ya watu kuhusu kuridhiwa kwa mkataba huo inayotokana na ushirikishwaji wa umma uliofanywa na Kamati husika; matokeo ya Kamati husika kuhusu mkataba huo na taarifa nyingine yoyote ambayo Kamati husika itachukulia kuwa muhimu; na pendekezo kwamba Bunge la Taifa liidhinishe uridhiaji wa mkataba huo, au liidhinishe uridhiaji wa mkataba huo bila ridhaa kamili, au likatae kuridhia mkataba huo.

Katika kuidhinisha uridhiaji wa mkataba bila ridhaa kamili, Bunge la Taifa litabainisha vipengele na mapendekezo kwa kila kipengele ambacho hakikuridhiwa kikamilifu yanayoweza kujumuisha maelekezo ya muda ambao wajibu mahususi unapaswa kutimizwa kabla ya kutekeleza mkataba huo.

Katika muda usiozidi siku saba kufuatia uamuzi wa Bunge la Taifa kuhusu mkataba, Katibu atamfahamisha waziri husika na Katibu atahifadhi taarifa hiyo katika sajili ya mikataba.

Idadi ya Kamati ya Kuratibu Shughuli za Bunge la Taifa kuongezwa hadi 14

Kanuni ya 171 imerekebishwa ili kuongeza idadi ya Kamati ya Kuratibu Shughuli za Bunge la Taifa hadi 14. Itakuwa na:

 • Spika ambaye atakuwa Mwenyekiti
 • Kiongozi wa Chama cha walio Wengi au mwakilishi wake aliyeteuliwa kimaandishi
 • Kiongozi wa Chama cha walio Wachache au mwakilishi wake aliyeteuliwa kimaandishi
 • Mratibu wa Chama cha walio Wengi au mwakilishi wake aliyeteuliwa kimaandishi
 • Mratibu wa Chama cha walio Wachache au mwakilishi wake aliyeteuliwa kimaandishi
 • Wabunge wengine tisa ambao watateuliwa na Vyama Bunge na kuidhinishwa na Bunge la Taifa mwanzoni mwa kila Kipindi, ikiakisi wingi wa idadi ya Wabunge wa kila Chama Bunge katika Bunge la Taifa na kuzingatia maslahi ya vyama visivyo Vyama Bunge na Wabunge Huru.

Maslahi ya vyama visivyo vyama bunge na Wabunge Huru yamezingatiwa

Maslahi ya vyama visivyo vyama bunge na Wabunge Huru yamezingatiwa katika kanuni ya 172, 173, 174 na 176.

Katika kanuni ya 172, Kamati ya Kuteua Wajumbe wa Kamati itakuwa na Kiongozi wa Chama cha walio Wengi atakayekuwa Mwenyekiti; Kiongozi wa Chama cha walio Wachache; na Wabunge wasiopungua kumi na mmoja na wasiozidi kumi na tisa watakaoteuliwa na Vyama Bunge na kuidhinishwa na Bunge la Taifa kwa kuzingatia maslahi ya vyama visivyo vyama bunge na Wabunge Huru.

Kanuni ya 173 inataja kwamba isipokuwa kama imeelezwa vinginevyo na sheria au Kanuni hizi, Kamati ya Kuteua Wajumbe wa Kamati, kwa kushauriana na Vyama Bunge, itateua Wajumbe watakaohudumu katika Kamati.

Kanuni ya 174 inataja kwamba Mbunge wa chama kisicho Chama Bunge au Mbunge Huru atateuliwa kuhudumu katika kamati moja na, kadri iwezekanavyo, idadi ya Wabunge katika kila Kamati ina uwiano na idadi ya Wabunge ambao ni wanachama wa vyama hivyo na Wabunge Huru.

Kanuni ya 176 inataja kwamba chama kinaweza kumwondoa mjumbe kwenye Kamati baada ya kumpa mjumbe huyo fursa ya kusikizwa. Pia, inataja kwamba Spika atamwondoa Mjumbe yeyote anayekiuka Kanuni ya 107A (Utovu Mkubwa wa Nidhamu) au anayevunja staha inayompasa Mbunge kutoka kwa Kamati ya Bunge la Taifa inayosimamia mamlaka na haki za Bunge la Taifa na mwenendo wa Wabunge.

Mbunge anaweza kukataa kuhudumu katika kamati ya Bunge la Taifa

Kwa mujibu wa Kanuni ya 173A, Mbunge anaweza kukataa kuhudumu katika kamati ya Bunge la Taifa  kwa kumwarifu Spika kwa maandishi.

Idadi ya wajumbe wa kamati kati ya 11-15

Kanuni ya 177 inaeleza kwamba  Kamati itakuwa na idadi witiri ya wajumbe ambayo haitapungua 11 na haitazidi 15.

Kanuni mpya inayoeleza mambo yatakayozingatiwa katika uteuzi wa Kamati inayosimamia haki na mwenendo wa Wajumbe

Kanuni mpya ya 177A inaeleza kwamba katika kuteua wajumbe wa kamati ya Bunge la Taifa inayosimamia mamlaka na haki za Bunge la Taifa na mwenendo wa Wabunge, Kamati ya Kuteua Wajumbe wa Kamati itazingatia—

 • wadhifa wa awali wa Mbunge katika Bunge la Taifa kama—

♦ Spika;

♦ Kiongozi wa Chama cha walio Wengi;

♦ Kiongozi wa Chama cha walio Wachache;

♦ Naibu Spika; au

♦ mjumbe wa Jopo la Mwenyekiti;

 • Mbunge aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi katika—

♦ Bunge la Taifa;

♦ Bunge la Taifa, Seneti na Bunge la Afrika Mashariki;

♦ Seneti; na

♦ Bunge la Afrika Mashariki;

 • elimu na weledi katika sheria, uandamizi katika utawala wa umma, upatanisho, usuluhishi, au atakavyobainisha Spika;
 • tajriba mahususi katika desturi na taratibu za Bunge; na
 • ukiukaji wowote wa Kanuni ya 107A (Utovu Mkubwa wa Nidhamu) au ukiukaji wa kanuni za maadili yanayomhusu Mbunge katika muhula wa Bunge.

Arifa za mikutano kielektroniki na kupitia nambari ya simu sasa inakubalika

Kanuni ya 181 inaeleza kwamba arifa ya mkutano itachukuliwa kuwa imetolewa pindi inaposambazwa kielektroniki kwa Mbunge kupitia anwani rasmi ya mawasiliano ya Mbunge au nambari yake ya simu, wavuti wa Bunge, kwa kufikishwa kwa ofisi ya Mbunge au kubandikwa kwenye maeneo ya Bunge.

Rekebisho la kanuni ya 183 ili kudhibiti uundaji, uanachama, akidi na majukumu ya kamati ndogo

Kanuni ya 183 imerekebishwa ili kudhibiti uundaji, uanachama, akidi na majukumu ya kamati ndogo.

Kanuni inataja kwamba Kamati inaweza kuunda kamati ndogo kadri itakavyoona ni muhimu kwa utekelezaji bora wa shughuli zake na kuagiza akidi isipungue wajumbe watatu. Iwapo akidi haitatimia katika muda wa dakika thelathini baada ya saa iliyopangwa, mkutano wa Kamati ndogo utaahirishwa hadi saa au siku nyingine itakayoamuliwa na Mwenyekiti wa Kamati.

Kazi ya Kamati ndogo itaendeshwa kwa mujibu wa maelekezo ya Kamati na hiyo Kamati ndogo itatoa ripoti mara kwa mara kwa Kamati kuhusu majukumu iliyopewa.

Huwezi kuondoa saini katika arifa ya kura ya kutokuwa na imani na Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti

Kanuni ya 193 imerekebishwa kwa kuchopeka aya inayoeleza kuwa pindi Katibu anapopata arifa kwa maandishi ya kura ya kutokuwa na imani na Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti, saini yoyote iliyotiwa kwenye arifa haitaondolewa.

Ripoti za utendakazi wa Kamati kuwasilishwa kila robo ya mwaka badala ya kila nusu ya mwaka

Hapo awali, ripoti za utendakazi wa kamati ulikuwa ukiwasilishwa kila nusu ya mwaka. Kutokana na rekebisho la Kanuni ya 200, ripoti inafaa kuwasilishwa kwa Kamati ya Kuratibu Shughuli za Kamati kila robo ya mwaka.

Ripoti za mwisho wa muhula kuwasilishwa na kila Kamati

Hapo awali, Kanuni ya 200A ilieleza kwamba “Kamati ambayo haingeweza kukamilisha kazi yake kabla ya mwisho wa muhula wake” ungewasilisha katika Bunge la Taifa ripoti ya mwisho wa muhula wake ikieleza sababu za kutoweza kukamilisha kazi iliyokabidhiwa.

Kutokana na rekebisho lilofanywa katika kanuni hii, jukumu hili ni la kila Kamati. Kanuni sasa inaeleza kwamba Mwenyekiti wa Kamati atawasilisha katika Bunge la Taifa ripoti ya mwisho wa muhula wake ikieleza kazi na mafanikio yoyote ya Kamati yake katika muhula huo na suala lolote linaloshughulikiwa na Kamati hiyo pamoja na sababu za kutolikamilisha kabla ya mwisho wa muhula wake.

Ripoti hiyo itakabidhiwa Kamati itakayofuata ambayo inaweza kuizingatia inapoandaa mpangokazi wake.

Idadi ya wajumbe wa Kamati ya Uteuzi kupunguzwa toka 28 hadi 21

Hapo awali, Kanuni ya 204 ilitaja kwamba Kamati ya Uteuzi itakuwa na Spika kama Mwenyekiti, Naibu Spika, Kiongozi wa Chama cha walio Wengi, Kiongozi wa Chama cha walio Wachache, Naibu Kiongozi wa Chama cha walio Wengi, Naibu Kiongozi wa Chama cha walio Wachache na Wabunge wengine wasiozidi ishirini na wawili watakaoteuliwa na Kamati ya Kuratibu Shughuli za Bunge la Taifa kwa kuzingatia nguvu katika wingi wa idadi ya Wabunge katika vyama vilivyowakilishwa katika Bunge la Taifa na maslahi ya Wabunge Huru.

Hivyo, idadi ya Kamati ya awali haingepita wajumbe 28.

Kanuni ya 204 imerekebishwa ili kupunguza idadi ya wajumbe wa Kamati hii kwa kueleza kuwa Kamati ya Uteuzi itakuwa na Spika kama Mwenyekiti, Naibu Spika, Kiongozi wa Chama cha walio Wengi, Kiongozi wa Chama cha walio Wachache, Naibu Kiongozi wa Chama cha walio Wengi, Naibu Kiongozi wa Chama cha walio Wachache na Wabunge wengine wasiozidi kumi na watano watakaoteuliwa na Kamati ya Kuratibu Shughuli za Bunge la Taifa kwa kuzingatia nguvu katika wingi wa idadi ya Wabunge katika vyama vilivyowakilishwa katika Bunge la Taifa na maslahi ya Wabunge Huru.

Kwa sasa, idadi ya Kamati haiwezi kupita wajumbe 21.

Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Umma kutoka Chama cha walio Wachache

Kanuni ya 205 imerekebishwa ili kueleza kuwa Kamati ya Hesabu za Umma itakuwa na Mwenyekiti kutoka Chama cha walio Wachache.

Kamati ya Hesabu za Umma itakayoundwa mara tu baada ya uchaguzi mkuu itahudumu kwa muda wa miaka mitatu ya kalenda na Kamati itakayoundwa baada yake itahudumu kwa muda uliosalia wa muhula wa Bunge hilo (miaka miwili).

Majukumu ya Kamati ya Hesabu za Hazina Maalum kupunguzwa na Kamati mpya (Kamati ya Hesabu za Hazina Tengwa) kuundwa

Kanuni ya 205A imerekebishwa ili kugawanya majukumu ya Kamati ya Hesabu za Hazina Maalum na Kamati ya Hesabu za Hazina Tengwa. Kamati ya Hesabu za Hazina Maalum itakagua ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu:

♦ Hazina zinazoundwa kisheria au kupitia sheria ndogo, isipokuwa Hazina kwa mujibu wa Kanuni ya 205B (Kamati ya Hesabu za Hazina Tengwa)

♦ Hazina ya Usawazishaji;

♦ Bodi ya Ushauri kwa Hazina ya Usawazishaji; na

♦ Hazina ya Vyama vya Kisiasa.

Rekebisho limeeleza pia kuwa mwanzoni mwa kila muhula wa Bunge au wakati mwingine wowote unaofaa, Spika atatoa orodha inayobainisha Hazina zinazohusiana na wajibu wa Kamati hiyo.

Aidha, Kamati ya Hesabu za Hazina Maalum itakayoundwa mara tu baada ya uchaguzi mkuu itahudumu kwa muda wa miaka mitatu ya kalenda na Kamati itakayoundwa baada yake itahudumu kwa muda uliosalia wa muhula wa Bunge hilo.

Kanuni mpya ya 205B imeunda Kamati ya Hesabu za Hazina Tengwa. Kamati hii itawajibika kukagua ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali za—

♦ Hazina ya Serikali ya Taifa kwa Maendeleo ya Maeneobunge;

♦ Bodi ya Hazina ya Serikali ya Taifa kwa Maendeleo ya Maeneobunge;

♦ Hazina ya Serikali ya Taifa kwa Hatua Sawazishi; na

♦ Bodi ya Hazina ya Serikali ya Taifa kwa Hatua Sawazishi.

Kamati hii itakuwa na Mwenyekiti atakayechaguliwa miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya vyama visivyounda Serikali ya Taifa na wajumbe wengine wasiozidi kumi na wanne.

Katika uanachama wa Kamati hii, vyama visivyo vyama bunge vinavyounda Serikali ya Taifa vitakuwa na mjumbe mmoja zaidi.

Kamati ya Hesabu za Hazina Tengwa haitakagua masuala ya sera au usimamizi wa kila siku wa hazina hizo maalum.

Kamati ya Hesabu za Hazina Tengwa itakayoundwa mara tu baada ya uchaguzi mkuu itahudumu kwa muda wa miaka mitatu ya kalenda na Kamati itakayoundwa baada yake itahudumu kwa muda uliosalia wa muhula wa Bunge hilo.

Kamati ya Uwekezaji wa Umma imegawanywa kuwa tatu: Kamati ya Uwekezaji wa Umma kuhusu Utawala na Elimu, Kamati ya Uwekezaji wa Umma kuhusu Masuala ya Kibiashara na Kawi, na Kamati ya Uwekezaji wa Umma kuhusu Huduma kwa Jamii, Usimamizi na Kilimo

Kamati ya Uwekezaji wa Umma imegawanywa kuwa tatu: Kamati ya Uwekezaji wa Umma kuhusu Utawala na Elimu, Kamati ya Uwekezaji wa Umma kuhusu Masuala ya Kibiashara na Kawi, na Kamati ya Uwekezaji wa Umma kuhusu Huduma kwa Jamii, Usimamizi na Kilimo.

Kamati hizi zitakuwa na Mwenyekiti kutoka Chama cha walio Wachache. Mwanzoni mwa kila muhula wa Bunge au wakati mwingine wowote unaofaa, Spika atatoa orodha inayobainisha mashirika ya umma yanayohusiana na wajibu wa Kamati kila moja ya Kamati hizi. Kamati hizi zinafaa kuhudumu kwa muhula miwili: muhula wa kwanza wa miaka mitatu na muhula wa pili wa miaka miwili. Pia, Kamati hizi zinapaniwa kuhudumu kwa miaka mitano kisha Bunge la Taifa linaweza kuamua kuziendeleza katika muhula mwingine wa Bunge la Taifa.

Kamati ya Uwekezaji wa Umma kuhusu Utawala na Elimu

Kanuni ya 206 inaunda Kamati ya Uwekezaji wa Umma kuhusu Utawala na Elimu. Katika kushughulikia masuala ya sekta za elimu, ulinzi, utawala, haki na uzingatiaji wa sheria, Kamati hii itachunguza ripoti na hesabu za uwekezaji wa umma; itachunguza ripoti, ikiwa zipo, za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu uwekezaji wa umma; na itachunguza, kwa kuzingatia uhuru na taratibu bora za uwekezaji wa umma, ili kubaini iwapo masuala yanayohusu uwekezaji wa umma yanasimamiwa kulingana na kanuni za kifedha au kibiashara pamoja na taratibu zinazofaa za kibiashara.

Kamati hii haitachunguza yafuatayo:

 • masuala ya sera muhimu ya Serikali ambayo hayahusiani na shughuli za biashara au uwekezaji wa umma;
 • masuala ya usimamizi wa kila siku; na
 • masuala ambayo utaratibu wa kuyashughulikia umewekwa katika sheria mahususi iliyoanzisha uwekezaji huo wa umma.

Kamati ya Uwekezaji wa Umma kuhusu Masuala ya Kibiashara na Kawi

Kanuni ya 206A imeunda Kamati ya Uwekezaji wa Umma kuhusu Masuala ya Kibiashara na Kawi. Katika kushughulikia masuala ya sekta za kawi, mazingira, masuala ya jumla ya kiuchumi na kibiashara, Kamati hii itachunguza ripoti na hesabu za uwekezaji wa umma; itachunguza ripoti, ikiwa zipo, za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu uwekezaji wa umma; na itachunguza, kwa kuzingatia uhuru na taratibu bora za uwekezaji wa umma, ili kubaini iwapo masuala yanayohusu uwekezaji wa umma yanasimamiwa kulingana na kanuni za kifedha au kibiashara pamoja na taratibu zinazofaa za kibiashara.

Kamati hii haitachunguza yafuatayo:

 • masuala ya sera muhimu ya Serikali ambayo hayahusiani na shughuli za biashara au uwekezaji wa umma;
 • masuala ya usimamizi wa kila siku; na,
 • masuala ambayo utaratibu wa kuyashughulikia umewekwa katika sheria mahususi iliyoanzisha uwekezaji huo wa umma.

Kamati ya Uwekezaji wa Umma kuhusu Huduma kwa Jamii, Usimamizi na Kilimo

Kanuni ya 206B imeunda Kamati ya Uwekezaji wa Umma kuhusu Huduma kwa Jamii, Usimamizi na Kilimo.

Katika kushughulikia masuala ya sekta za kilimo, usimamizi wa umma, afya, na maslahi ya kijamii, Kamati hii itachunguza ripoti na hesabu za uwekezaji wa umma; itachunguza ripoti, ikiwa zipo, za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu uwekezaji wa umma; na itachunguza, kwa kuzingatia uhuru na taratibu bora za uwekezaji wa umma, ili kubaini iwapo masuala yanayohusu uwekezaji wa umma yanasimamiwa kulingana na kanuni za kifedha au kibiashara pamoja na taratibu zinazofaa za kibiashara.

Kamati hii haitachunguza yafuatayo:

 • masuala ya sera muhimu ya Serikali ambayo hayahusiani na shughuli za biashara au uwekezaji wa umma;
 • masuala ya usimamizi wa kila siku; na,
 • masuala ambayo utaratibu wa kuyashughulikia umewekwa katika sheria mahususi iliyoanzisha uwekezaji huo wa umma.

Kamati ya Deni la Umma na Ubinafsishaji (Kamati mpya)

Kanuni ya 207A imeunda Kamati mpya inayoitwa Kamati ya Deni la Umma na Ubinafsishaji.

Majukumu ya Kamati

Kamati hii itawajibikia:

♦ uangalizi wa deni la umma na dhamana kwa mujibu wa Ibara ya 214 ya Katiba

♦ uchunguzi wa masuala kuhusu dhamana za madeni ya Serikali ya Taifa

♦ uangalizi wa huduma zilizogharimiwa na Hazina Kuu isipokuwa hesabu zilizokaguliwa

♦ uchunguzi wa ripoti za hali ya uchumi kuhusiana na deni la umma

♦ uangalizi wa miradi inayotokana na Ushirikiano kati ya Umma na Sekta ya Kibinafsi inayotekelezwa na Serikali ya Taifa kuhusiana na deni la umma

♦ uangalizi wa ubinafsishwaji wa rasilimali za taifa

Kuhusu deni la taifa, Kamati hii:

♦ itazingatia na kukagua masharti ambayo yataongoza ukopaji wa Serikali ya Taifa ikiwa ni pamoja na upeo wa kukopa

♦ itachunguza kiasi cha deni la taifa;

♦ itachunguza matumizi yaliyofanywa au yatakayofanywa kutokana na mapato ya mikopo ya taifa na dhamana za Serikali ya Taifa;

♦ itachunguza taratibu zilizowekwa kushughulikia au kulipia mikopo na dhamana za taifa;

♦ itachunguza Mkakati wa Kudhibiti Deni wa kila mwaka kwa muda wastani utakaowasilishwa katika Bunge la Taifa na waziri anayehusika na masuala ya fedha;

♦ itachunguza hatua zilizofikiwa katika ulipaji wa mikopo ya taifa na mikopo iliyodhaminiwa na Serikali ya Taifa;

♦ itatathmini na kuchunguza mapendekezo ya Serikali ya Taifa kuhusu mikopo na dhamana kwa serikali ya kaunti kwa mujibu wa Ibara ya 212(a) ya Katiba;

♦ itachunguza ripoti za kila mwaka zilizowasilishwa katika Bunge la Taifa kwa mujibu wa Ibara ya 213(2) ya Katiba kuhusu dhamana zilizotolewa na Serikali ya Taifa;

♦ itachunguza ripoti za kila robo ya mwaka zilizowasilishwa na Waziri katika Bunge kuhusu mikopo yote kwa Serikali ya Taifa, asasi za Serikali ya Taifa na serikali za kaunti kwa mujibu wa Ibara ya 211(2) ya Katiba;

♦ itatathmini sheria na masharti ya Serikali ya Taifa ya kudhamini mikopo;

♦ itatathmini uzingatiaji wa kanuni ya usawa kati ya vizazi katika ukopaji wa umma;

♦ itatathmini uzingativu wa Serikali ya Taifa kwa Katiba au sheria zinazohusiana na ukopaji wa umma na dhamana; na

♦ itachunguza ripoti zilizowasilishwa na waziri kuhusu dhamana za mikopo kwa biashara ndogondogo, ndogo na za wastani.

Ripoti za Kamati, Mwenyekiti, Muhula

Kamati hii itatoa ripoti na mapendekezo kwa Bunge la Taifa mara kwa mara itakavyowezekana, ikijumuisha mapendekezo ya sheria kwa masuala yanayohusu wajibu wake. Pia, Kamati hii itakuwa na Mwenyekiti kutoka kwa Chama cha walio Wachache.

Kamati ya Deni la Umma na Ubinafsishaji itakayoundwa mara tu baada ya uchaguzi mkuu itahudumu kwa muda wa miaka mitatu ya kalenda na Kamati itakayoundwa baada yake itahudumu kwa muda uliosalia wa muhula wa Bunge hilo (miaka miwili).

Idadi ya Wajumbe wa Kamati ya Utaratibu na Kanuni za Bunge la Taifa imepunguzwa

Kanuni ya 208 imerekebishwa ili kupunguza idadi ya Wajumbe wa Kamati ya Utaratibu na Kanuni za Bunge la Taifa hadi 21. Kanuni inataja kwamba Kamati hii itakuwa na Spika kama Mwenyekiti, Naibu Spika, wajumbe wa Jopo la Mwenyekiti na Wabunge wengine wasiozidi kumi na watatu.

Kamati ya Utaratibu na Kanuni za Bunge la Taifa itakayoundwa mara tu baada ya uchaguzi mkuu itahudumu kwa muda wa miaka mitatu ya kalenda na Kamati itakayoundwa baada yake itahudumu kwa muda uliosalia wa muhula wa Bunge hilo (miaka miwili).

Mabadiliko kuhusu ardhilhali za umma

Kanuni mpya ya 208A imeunda Kamati ya Ardhilhali za Umma.

Majukumu ya Kamati ya Ardhilhali za Umma

 • Kushughulikia ardhilhali zote za umma zilizowasilishwa katika Bunge la Taifa
 • Kutoa mapendekezo inavyofaa kuhusu maombi ya ardhilhali hizo
 • Kupendekeza iwapo matokeo yanayotokana na kushughulikia ardhilhali yanafaa kujadiliwa
 • Kushauri Bunge la Taifa na kuripoti kuhusu ardhilhali zote za umma ilizokabidhiwa

Haya ni mabadiliko mengine:

 • mwenye Ardhilhali anapaswa kuambatisha ushahidi wa juhudi zilizofanywa ili masuala yanayoibuliwa kwenye Ardhilhali yashughulikiwe na asasi husika  na pale ambapo masuala yangali kortini, ataambatisha ushahidi wa kusikilizwa au uamuzi. Hii ni kwa mujibu wa rekebisho lilofanywa katika Kanuni ya 223.
 • Kanuni ya 224 imefutwa. Ilikuwa inataja kwamba muda utakaotumika kwa ajili ya Shughuli ya “Ardhilhali” hautazidi dakika thelathini. Hivyo basi, Bunge la Taifa litakuwa na nafasi ya kujadili ardhilhali za umma.
 • Ardhilhali zote zitawasilishwa au kukabidhiwa Kamati ya Ardhilhali za Umma. Kabla ya rekebisho la Kanuni ya 227, ardhilhali ingekabidhiwa Kamati ya Kiidara inayohusika.
 • Muda wa Kamati kushughulikia Ardhilhali umeongezwa toka siku 60 hadi siku 90. Hii ni kutokana na rekebisho la Kanuni ya 227.

Kamati ya Masuala ya Ughaibuni na Wafanyakazi Wahamiaji (Kamati mpya)

Kanuni ya 208B imeunda Kamati ya Ughaibuni na Wafanyakazi Wahamiaji.

Majukumu ya Kamati ya Masuala ya Ughaibuni na Wafanyakazi Wahamiaji

 • Kushughulikia masuala yote ambayo moja kwa moja yanahusu sera na mipango ya kulinda haki na ustawi wa Wakenya walio ughaibuni, ikijumuisha raia wa Kenya wenye uraia wa nchi mbili; wakenya wahamiaji wanaofanya kazi nje ya nchi pamoja na familia zao ughaibuni; na wakenya wanaosomea ughaibuni.
 • Kutathmini sera na mipango ya Serikali ya Taifa kuhusu:

♦ kuvutia kwa namna bora, kuleta pamoja na kutumia kwa njia inayofaa rasilimali za Kenya ughaibuni kwa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni

♦ kuwashirikisha na kuwawezesha Wakenya walio ughaibuni, pamoja na watu wanaostahiki kupata uraia wa nchi mbili

♦ haki ya Wakenya walio ughaibuni kupiga kura

Idadi za wajumbe wa Kamati hizi kupunguzwa hadi 21: Kamati ya Utekelezaji, Kamati ya Utangamano wa Kikanda, Kamati ya Mshikamano wa Kitaifa na Fursa Sawa na Kamati ya Utangazaji wa Shughuli za Bunge na Maktaba

Idadi za wajumbe wa Kamati hizi Kamati imepunguzwa hadi 21: Kamati ya Utekelezaji, Kamati ya Utangamano wa Kikanda, Kamati ya Mshikamano wa Kitaifa na Fursa Sawa na Kamati ya Utangazaji wa Shughuli za Bunge na Maktaba

Hii ni kutokana na marekebisho ya Kanuni hizi:

Kanuni ya 209 (Kamati ya Utekelezaji), Kanuni ya 212 (Kamati ya Utangamano wa Kikanda), Kanuni ya 212C(Kamati ya Mshikamano wa Kitaifa na Fursa Sawa) na Kanuni ya 212D( Kamati ya Utangazaji wa Shughuli za Bunge na Maktaba).

Marekebisho kuhusu  Kamati ya Sheria Ndogo

Marekebisho yaliyofanywa katika Kanuni ya 210 kuhusu Kamati ya Sheria Ndogo ni yafuatayo:

 • Kamati hii itakuwa na Mwenyekiti na Wajumbe wengine wasiozidi ishirini (Aya mpya ya 1A)
 • Kamati hii, katika kila robo ya mwaka, itawasilisha ripoti kwa Bunge la Taifa yenye orodha ya sheria ndogo zilizoidhinishwa (Aya mpya ya 5A)
 • Pale ambapo Bunge la Taifa linabatilisha sehemu ya sheria ndogo au sheria ndogo yote, mamlaka iliyotunga sheria hiyo itamuarifu Katibu na kuwasilisha ushahidi wa kuchapishwa kwa kubatilishwa huko katika muda usiozidi siku ishirini na moja. (Aya mpya ya 5B)
 • Katibu atahifadhi taarifa alizopokea kwa mujibu wa aya ya (5B) katika sajili ya sheria ndogo na kuiwasilisha kwa Kamati. (Aya mpya ya 5C)
 • Kamati ya Sheria Ndogo itakayoundwa mara tu baada ya uchaguzi mkuu itahudumu kwa muda wa miaka mitatu ya kalenda na Kamati itakayoundwa baada yake itahudumu kwa muda uliosalia wa muhula wa Bunge hilo. (Aya mpya ya 5D)

Kamati ya Kuteua Wajumbe wa Kamati kuzingatia maslahi ya Vyama visivyokuwa Vyama Bunge na Wabunge Huru katika kuteua wabunge watakaohudumu kwenye Kamati ya Pamoja

Kanuni ya 213(3) imerekebishwa na inataja kwamba Wabunge watakaohudumu kwenye Kamati ya Pamoja watateuliwa na Kamati ya Kuteua Wajumbe wa Kamati kwa kushauriana na Vyama Bunge, Vyama visivyokuwa Vyama Bunge na Wabunge Huru mwanzoni mwa muhula wa Bunge.

Marekebisho kuhusu idadi wa wajumbe katika Kamati za Kiidara na majukumu

Kanuni 216 imefanyiwa marekebisho kadhaa. Mwanzo, wajumbe wa Kamati za Kiidara watateuliwa na Kamati ya Kuteua Wajumbe wa Kamati ikishauriana na vyama Bunge, Vyama visivyokuwa Vyama Bunge na Wabunge Huru mwanzoni mwa muhula wa kila Bunge. Hapo awali, Vyama visivyokuwa Vyama Bunge na Wabunge Huru havikushauriwa. Pili, Wajumbe wa Kamati za Kiidara wamepunguzwa toka 19 hadi 15. Tatu, Kamati za Kiidara zimeongezewa jukumu la kufuatilia na kuwasilisha ripoti ya utekelezaji wa bajeti ya kitaifa kulingana na wajibu wake kila robo ya mwaka.

Taarifa ya kutosha kutolewa wakati Bunge la Taifa linashughulikia makadirio katika Kamati ya Ugavi wa Fedha

Kanuni ya 235 imerekebishwa na aya mpya ya (6) kuchopekwa. Aya hii inataja kwamba pale ambapo Kamati ya Bajeti na Uidhinishaji wa Matumizi inapendekeza mabadiliko yoyote au ugawaji upya katika Makadirio, Kamati ya Bajeti na Uidhinishaji wa Matumizi itajumuisha katika mapendekezo yake jedwali linaloonyesha mabadiliko au ugawaji upya unaopendekezwa kwa kila Fungu, Fungu Dogo, Mpango, Mradi, Matokeo Tarajiwa au Lengo. Habari hii ni muhimu ili kusaidia Wabunge wafanye uamuzi wa busara.

Uwazi katika uidhinishaji wa matumizi

Kanuni mpya ya 240B inashughulikia Mswada wa Kuidhinisha Matumizi  ya Fedha na Mswada wa Kuidhinisha Matumizi ya Fedha ya Hazina ya Usawazishaji.

Kanuni hii inataja kwamba uamuzi wa Bunge la Taifa kwenye Makadirio ya Bajeti na Makadirio ya Matumizi kutoka kwa Hazina ya Usawazishaji utatumika kama msingi wa kuandaa Mswada wa Kuidhinisha Matumizi ya Fedha na Mswada wa Kuidhinisha Matumizi ya Fedha ya Hazina ya Usawazishaji.

Baada ya makadirio ya bajeti kuidhinishwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Uidhinishaji wa Matumizi atawasilisha katika Bunge la Taifa Mswada wa Kuidhinisha Matumizi ya Fedha na, iwapo itahitajika, Mswada wa Kuidhinisha Matumizi ya Fedha ya Hazina ya Usawazishaji.

Bunge la Taifa litashughulikia marekebisho yoyote yatakayopendekezwa kwenye Mswada wa Kuidhinisha Matumizi  ya Fedha kwa kuzingatia mapendekezo ya Kamati ya Bajeti na Uidhinishaji wa Matumizi baada ya kushauriana na kamati za kiidara zinazohusika.

Bunge la Taifa litashughulikia na kupitisha Mswada wa Kuidhinisha Matumizi Fedha na isiwe baada ya tarehe 26 Juni kila mwaka.

Baada ya kupitishwa kwa Mswada wa Kuidhinisha Matumizi ya Fedha, haraka iwezekanavyo, Katibu atathibitisha kwa maandishi marekebisho yoyote yaliyofanywa kwa Fungu au Mpango na ataonyesha ugawaji upya, nyongeza au mapunguzo yaliyofanywa na Bunge la Taifa kwa Fungu, Fungu Dogo, Mpango, Mradi, Matokeo Tarajiwa au Lengo kumwezesha Waziri anayehusika na masuala ya fedha kuchapisha Makadirio ya mwisho yaliyoidhinishwa.

Kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Kuidhinisha Matumizi ya Fedha, Kamati ya Bajeti na Uidhinishaji wa Matumizi itahakikisha kwamba ugawaji upya wowote, nyongeza au mapunguzo yaliyofanywa na Bunge la Taifa katika Makadirio kwa kila Fungu, Fungu Dogo, Mpango, Mradi, Matokeo Tarajiwa au Lengo yanajumuishwa kwenye vitabu vya bajeti vya mwisho ambavyo vitachapishwa tena.

Marekebisho kwenye Bajeti ya Ziada ili ioane na ibara ya 223 ya Katiba

Kanuni ya 243 imefanyiwa marekebisho kadhaa.

Kanuni sasa inaeleza kwambaBajeti ya Ziada itajumuisha yafuatayo (zaidi ya mengine katika Kanuni):

 • sababu na stakabadhi za kifedha kama ushahidi wa pesa zilizotumiwa
 • nyongeza tofauti kwa matumizi yaliyofanywa kwa mujibu wa Ibara ya 223 ya Katiba na ugawaji upya wowote uliofanywa katika Fungu lolote
 • nyongeza inayoonyesha pesa zilizotumiwa na sababu ya pesa hizo kutumiwa katika kila Fungu, Mpango au Mradi
 • tarehe ambapo pesa hizo zilitolewa kwa mara ya kwanza

Aya mpya ya 3A inaeleza kwamba ripoti ya Kamati ya Bajeti na Uidhinishaji wa Matumizi kwa Bunge la Taifa kuhusu Makadirio ya Ziada:

 • itajumuisha tathmini ya uzingativu wa mapendekezo ya Makadirio ya Ziada kwa masharti yaliyoorodheshwa katika Ibara ya 223 ya Katiba na sheria nyingine yoyote; na kanuni na maadili ya fedha za umma kwa mujibu wa Ibara ya 201 ya Katiba
 • itakuwa na vipengele pekee vya pesa ambazo tayari zimetolewa na kutumiwa na Serikali ya Kitaifa kwa mujibu wa Ibara ya 223 ya Katiba
 • itakuwa na nyongeza tofauti ya matumizi yaliyofanywa kwa mujibu wa Ibara ya 223 ya Katiba na ugawaji upya wowote wa kawaida uliofanywa katika fungu lolote na nyongeza ya fedha au maamuzi ya sera.

Aya mpya ya 3B inaeleza kwamba Aya ya 3A itatumika kwa Kamati ya Kiidara inayotathmini Makadirio ya Ziada na kutoa mapendekezo kwa Kamati ya Bajeti na Uidhinishaji wa Matumizi kwa mujibu wa Kanuni ya 243(3).

Aya mpya ya 3C inataja kwamba Katibu atahifadhi sajili mahususi ya kurekodi maombi yoyote ya idhini yanayofanywa na Waziri anayehusika na fedha kwa mujibu wa Ibara ya 223 ya Katiba na atahakikisha maombi hayo yanawasilishwa katika Bunge la Taifa kwa muda unaofaa.

Kanuni mpya kuhusu ufuatiliaji wa utekelezaji wa bajeti

Kanuni mpya ya 245A inaeleza utaratibu wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa bajeti.

Mwanzo, knuni hii inataja kwamba katika kutathimini utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ya Taifa, Kamati ya Bajeti na Uidhinishaji wa Matumizi:

 • itahakiki ripoti za kila robo ya mwaka zinazowasilishwa na Waziri anayehusika na masuala ya fedha kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma
 • itahakiki ripoti zinazowasilishwa na Msimamizi wa Bajeti ambazo zinahusu utekelezaji wa Bajeti kuhusiana na Bunge na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
 • itatathmini na kuripoti kuhusu matumizi na utendakazi usio wa kifedha wa Bajeti ya Bunge na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
 • itatathmini utimilifu wa mchakato wa utekelezaji kwa misingi ya kanuni na maadili ya fedha za umma kama inavyoelezwa na Ibara ya 201 ya Katiba
 • itahakikisha iwapo rasilimali zozote mpya zinazotoka kwa mapato ya kodi na ruzuku zilizokusanywa na Serikali ya Taifa katika mwaka zinatumiwa kupunguza nakisi ya fedha.

Pili, katika kufuatilia na kuwasilisha ripoti ya utekelezaji wa bajeti ya kitaifa kulingana na wajibu wake kila robo ya mwaka, kila Kamati ya Kiidara:

 • itatathmini ripoti za kila robo ya mwaka zilizowasilishwa na Waziri anayehusika na masuala ya fedha kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma
 • itachanganua ripoti zilizowasilishwa na Msimamizi wa Bajeti ambazo zinahusu masuala ya utekelezaji wa Bajeti kuhusiana na Serikali ya Taifa
 • itatathmini na kuripoti kuhusu matumizi na utendakazi usio wa kifedha wa Bajeti ya Serikali ya Taifa
 • itatathmini utimilifu wa mchakato wa utekelezaji kwa misingi ya kanuni na maadili ya fedha za umma kama inavyoelezwa na Ibara ya 201 ya Katiba.

Taarifa rasmi ya vikao vya Kamati za Bunge la Taifa kutolewa

Kanuni ya 248 imerekebishwa kwa kuchopeka aya mpya ya 1A inayoeleza kwamba taarifa ya neno kwa neno ya vikao vya Kamati za Bunge la Taifa pale ambapo ushahidi unatolewa itachapishwa katika muda usiozidi saa sabini na mbili isipokuwa pale ambapo Spika ameridhika kwamba haiwezekani kwa sababu ya tukio la dharura.

Masuala ya siri au ya kibinafsi kuondelewa kwenye Taarifa Rasmi za Kamati za Bunge la Taifa

Kanuni ya 249 imefanyiwa marekebisho ili kuondoa masuala ya siri au ya kibinafsi kwenye Taarifa Rasmi za Kamati za Bunge la Taifa. Kanuni hii sasa inataja kwamba Spika anaweza kuagiza kuondolewa kwenye Majarida ya Bunge la Taifa na Taarifa Rasmi ya Bunge la Taifa na Kamati zake suala lolote ambalo kwa maoni yake ni la siri au la kibinafsi na kuagiza liwekwe kwenye Taarifa Rasmi tofauti ambayo itahifadhiwa na Katibu na kuwekwa wazi kwa Wabunge pekee.

Upeperushaji wa matangazo ya shughuli za Kamati

Awali, kwa mujibu wa Kanuni ya 250, upeperushaji wa shughuli za Bunge la Taifa ulikuwepo.

Kupitia marekebisho ya Kanuni hii, upeperushaji wa matangazo ya shughuli za Kamati sasa unaruhusiwa.

Taratibu za shahidi kutoa ushahidi bila kuhusisha umma

Kanuni ya 252 inaeleza masharti ya jumla ya kuingia kwenye Bunge la Taifa. Kanuni hii imerekebishwa kupitia kuchopekwa kwa aya mpya mbili za 2A na 2B.

Aya mpya ya 2A inaeleza kwamba mtu anayehitajika kujiwasilisha mbele ya Kamati ya Bunge la Taifa anaweza kuomba kwa maandishi kwamba umma usiruhusiwe kuingia katika kikao atakachojiwasilisha angalau saa ishirini na nne kabla ya kujiwasilisha.

Aya mpya ya  2B inataja kwamba Kamati italifikiria ombi lililotolewa kwa mujibu wa aya ya (2A) kwa kuzingatia mahitaji ya Ibara ya 118 ya Katiba ya kuruhusu umma kuingia katika Bunge na maslahi ya umma, na kila mara Kamati inapokubali ombi kama hilo italiarifu Bunge la Taifa na kutoa sababu za kulikubali.

Kutambuliwa kwa Kikundi cha Wabunge Huru

Kanuni mpya ya 259B inaeleza kuwa kufuatia ombi la kimaandishi la angalau Wabunge Huru kumi, Spika anaweza kutambua kikundi cha Wabunge Huru kilichoundwa kwa minajili ya kuwawezesha Wabunge Huru kutekeleza majukumu yao katika Bunge la Taifa. Ombi kwa Spika kwa mujibu wa Kanuni hii litakuwa na majina na saini za Wabunge wa kikundi hicho. Kwa mujibu wa Kanuni hii, Spika atatambua kikundi kimoja pekee.

Kamati za Muda zinaweza kuundwa

Kanuni mpya ya 259C inataja kwamba baada ya kupata idhini kutoka kwa Kamati ya Kuratibu Shughuli za Bunge la Taifa, Mbunge anaweza kutoa hoja inayopendekeza kuundwa kwa Kamati ya Muda kuhusu suala maalum na la kipekee ambalo kwa wakati huo halishughulikiwi na Kamati ya Bunge la Taifa.

Hoja ya kuundwa kwa Kamati ya Muda inakuwa na nini?

♦ itataja jina linalopendekezwa kuwa la kamati hiyo

♦ itaeleza wajibu unaopendekezwa na upekee wa suala litakaloshughulikiwa na Kamati hiyo

♦ itafafanua uanachama na uongozi unaopendekezwa wa Kamati hiyo

Mambo ambayo Mtoahoja anafaa kuhakikisha

♦ uanachama wa Kamati hiyo unaopendekezwa unaakisi wingi wa Wabunge wa kila Chama Bunge katika Bunge la Taifa na unazingatia maslahi ya vyama ambavyo sio Vyama Bunge na Wabunge Huru

♦ uanachama unaopendekezwa kwa Kamati hiyo hauna zaidi ya thuluthi mbili ya wajumbe wa jinsia moja.

Isipokuwa Bunge la Taifa liamue vyinginevyo, Kamati ya Muda itashughulikia suala inalowajibikia na kutoa ripoti yake katika muda usiozidi siku 90.

Risala za Bunge la Taifa

Kanuni mpya ya 259D inataja kwamba Spika ataripoti kwa Bunge la Taifa kifo cha mtu ambaye, kwa maoni ya Spika, ni muhimu Bunge la Taifa kuarifiwa na risala za Bunge la Taifa zinaweza kutolewa kupitia kwa hoja ya kipekee.

Kwa idhini ya Spika, Mbunge anaweza kuripoti kifo cha Mbunge wa zamani; au kuarifu Bunge la Taifa kuhusu mafanikio ya kipekee ya Mkenya katika ngazi ya kitaifa, kikanda au kimataifa.

Spika anaweza kuwaruhusu Wabunge kutoa maoni kwa ufupi baada ya ripoti au arifa kutolewa kwa mujibu wa Kanuni hii.

Katibu atawasilisha nakala iliyothibitishwa ya Taarifa Rasmi kwa familia ya mtu ambaye Bunge la Taifa limemtolea risala.

Bunge la Taifa kupendekeza au kuteua maafisa kwa Ofisi za Umma

Kanuni mpya ya 259E inaeleza kwamba pale ambapo sheria au sheria ndogo inahitaji Bunge la Taifa kumpendekeza mtu kuteuliwa au kuteua mtu katika ofisi ya umma, Spika anaweza, ikiwa hakuna mwongozo, kutoa mwongozo wa jinsi uteuzi huo utafanywa.

Wasifu na Sajili ya Wabunge

Kanuni mpya ya 259F inataja kwamba mwanzoni mwa kila Bunge au baada ya uchaguzi mdogo, Mbunge atawasilisha kwa Katibu wasifu wake kwa njia inayoelekezwa kwenye Nyongeza ya Kumi kwa minajili ya kumwezesha Mbunge huyo katika masuala ya Bunge la Taifa na kuufahamisha umma.

Wakati wowote katika muhula wa Bunge, Mbunge anaweza kusasisha taarifa aliyotoa. Katibu atahifadhi wasifu wa Wabunge na mara kwa mara kusasisha taarifa hiyo kila wakati Mbunge anapowasilisha taarifa na anaweza kuchapisha taarifa hizo kwenye wavuti wa Bunge. Mbunge atawajibikia usahihi wa taarifa anayotoa.

Angalau mwezi mmoja kabla ya muhula wa Bunge kumalizika, Katibu atachapisha kwenye Gazeti Rasmi la Serikali, sajili ya Wabunge waliohudumu kwenye Bunge hilo kwa kufuata mpangilio wa kialfabeti.

Utambuzi wa Wabunge wenye Hadhi

Kanuni mpya ya 259G inaeleza kwamba mara kwa mara, Spika anaweza kumtambua na kumtaja Mbunge wa Bunge la Taifa kuwa Mbunge mwenye Hadhi.

Katika kumteua Mbunge mwenye Hadhi, Spika atazingatia  huduma ya awali ya Mbunge huyo katika Bunge la Taifa kama Spika, Naibu Spika, Kiongozi wa Chama cha Walio Wengi, au Kiongozi wa Chama cha Walio Wachache; na jumla ya muda ambao Mbunge huyo alihudumu katika Bunge la Taifa. Spika atamwarifu Mbunge huyo na Bunge la Taifa kuhusu haki zinazoambatana na uteuzi huo.

_

ayes & nays

Spread the love